banner

February 25, 2017

BARABARA ZA JUU KUANZA KUJENGWA UBUNGO

BARABARA ZA JUU KUANZA KUJENGWA UBUNGO

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wametiliana saini na Kampuni ya M/S China Civil Engineering Construction Cooperation ya China (CCECC) kwa ajili ya mkataba wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Sam Nujoma na Mandela eneo la Ubungo jijini Dar es Salaam, unaotarajiwa kugharimu zaidi ya Sh bilioni 177.4.
Mkataba huo uliosainiwa jana jijini Dar es Salaam, unamtaka mkandarasi Kampuni ya CCECC kutoka China kuanza ujenzi huo mara moja na ujenzi huo unatarajiwa kutumia takriban miezi 30 hadi kukamilika kwake.
Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara, Patrick Mfugale alisema zaidi ya Sh bilioni 177.4 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi huo, utakaowekewa jiwe la msingi mwezi ujao.
“Hakikisheni mnaanza ujenzi mara moja kwani serikali imeshakamilisha taratibu zote na tayari kiasi cha shilingi bilioni 2.1 kimelipwa kwa ajili ya fidia kwa wananchi walioguswa na mradi huo,” alieleza Mfugale.
Alisema ujenzi wa ‘Ubungo Interchange’ unajengwa kwa fedha ya mkopo kutoka Benki ya Dunia, na serikali kwa upande wake imeshalipa fidia ya zaidi ya Sh bilioni 2.1
“Zaidi ya magari 65,000 yanapita kila siku katika katika makutano ya barabara za Morogoro, Mandela na Sam Nujoma eneo la Ubungo, hali inayosababisha msongamano katika barabara ya Morogoro ambayo ndio lango kuu la kuingia na kutoka jijini Dar es Salaam,” alifafanua mtendaji huyo.
Alisema kutokana na hilo, ufanisi wa mradi huo utahuisha hali ya usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Mfugale alisema upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa ‘Ubungo Interchange’, ulifanywa na Kampuni ya M/S Hamza Associates ya Misri kwa kushirikiana na Kampuni ya Advanced Engineering Solutions Ltd ya Tanzania kwa gharama za dola za Marekani 440,540 sawa na Sh 951, 218,373.40 na kazi hiyo ilikamilika Desemba mwaka jana.
Aidha, alisema Mhandisi Mshauri kwa ajili ya usimamizi wa kazi ya ujenzi wa mradi huo ni Kampuni ya M/S DASAN Consultants ya Korea Kusini ikishirikiana na Kampuni ya AFRISA Consulting Ltd ya Tanzania, ambapo gharama za usimamizi ni Sh 8,286,234,524.
Alisema kulingana na usanifu, barabara za juu katika eneo la Ubungo zitajengwa kwa safu tatu, ambapo safu ya chini itatumika kwa magari yanayopita katika barabara ya Morogoro na magari yote yanayopinda kushoto.
Safu ya pili itajengwa katika urefu wa meta 5.75 kutoka usawa wa ardhi na itatumika kwa magari yote yanayopinda kulia ambayo yataongozwa pia na taa za barabarani.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search