banner

February 24, 2017

DC AAGIZA WENYE VIBANDA VYA KUBET WAKAMATWE

DC AAGIZA WENYE VIBANDA VYA KUBET WAKAMATWE

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam, Ali Hapi ameiagiza Ofisi ya Biashara ya Manispaa hiyo kushirikiana na Polisi kufanya operesheni katika vibanda vya michezo ya kubashiri “betting” na kuwakamata wanaowaruhusu watoto kushiriki michezo hiyo.
Mbali na kuwakamata wamiliki hao, pia amemuagiza Ofisa Biashara wa Manispaa hiyo, Mohamed Basama kuwasiliana na watoa leseni za mchezo huo Bodi ya Michezo ya Kubahatisha kuhakikisha wanafuta leseni za wote watakaobainika kuwaruhusu watoto kucheza mchezo huo.
Agizo hilo limekuja baada ya mkuu huyo wa wilaya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuwa watoto wao wamekuwa wakishindwa kusoma na wengine kujihusisha na wizi ili wapate fedha za kubeti.
Alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakishinda katika vibanda vya kubeti kuanzia asubuhi hadi usiku, hivyo kusababisha washindwe kuzingatia masomo yao shuleni.
"Fanyeni operesheni mkikuta watoto katika hayo mabanda ya kubeti, wakamateni wamiliki wa hayo mabanda mmuwasiliane na idara inayohusika kutoa leseni, mfute leseni zao na hiyo ndiyo dawa," alisema Hapi.
Aidha, alisema wapo watoto wengine wamekuwa wakishinda kwenye sehemu zinazoendesha michezo ya kamari kinyume na sheria, ambapo aliagiza pia watu hao wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Hapi alionya kama wazazi wasipokuwa makini kutoa taarifa juu ya vibanda ambavyo watoto wanaingia kushiriki mchezo huo, watatengeneza kizazi cha wajinga, kitu ambacho hawatakiwi kuruhusu kitokee.
“Unakuta watoto wanaingia darasani lakini vichwani mwao inapita mashine za kubeti tu, hata ukimuuliza saba mara mbili ngapi hajui. Tena wengine wana madude feki, mkiyakuta ng'oeni na muwapeleke nayo mahakamani hivyo ndio vidhibiti," alisema.
Awali akijibu malalamiko hayo, Basama alisema wamekuwa na changamoto kutokana na kwamba wao hawahusiki na utoaji wa leseni za biashara hizo na kuahidi watafanyia kazi maagizo ya mkuu huyo wa wilaya.
Akitoa malalamiko katika mkutano huo uliofanyika Kata ya Kinondoni, mkazi wa mtaa huo aliyejitambulisha kwa jina la Sophia alisema, watoto wao wamekuwa hawafiki shule na badala yake kuishia katika maeneo hayo.
“Yaani hata hela zetu ndani hazikai, ukiweka hela kidogo tu unakuta haipo ameshachukua anaenda kubeti, mheshimiwa tunaomba utoe maagizo kuhusu hii michezo ya kubeti ni hasara kwa watoto wetui," alisema mkazi huyo.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search