banner

February 26, 2017

HILO GOLI LA KICHUYA SI LA NCHI HII

HILO GOLI LA KICHUYA SI LA NCHI HII

USWAHILINI wanasema kapiga mwezi mchanga. Shiza Kichuya, goli lake alilowapiga Yanga jana Jumamosi hapo Taifa siyo la nchi hii. Unajua ilikuwaje?...Alichukua mpira hapo kati, akakimbia nao kulia kama anamfuata Mwinyi Haji akasita, halafu akakata kushoto.
Baada ya hapo tu akaugonga mpira mara ya kwanza, mabeki wa Yanga wamezubaa...akaugonga tena, wameendelea kuzubaa na kipa naye akazubaa akapiga mwezi mchanga.
Unaambiwa aliachia kitu kikapenya kwenye nyavu ndogo. Yanga wengine wakashika vichwa, wengine mikono shavuni ndio biashara ikaishia hapo. Hii ni mara ya pili mfululizo Kichuya anawanyima raha Yanga kwani kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi, alichomoa bao dakika ya 90 kwa kona ya moja kwa moja na mechi kumalizika kwa sare ya bao 1-1. Achana na hayo, jana Yanga ilikufa kwa dakika 14 tu.
Kwani Simba walichomoa kwa bao la kichwa cha Laudit Mavugo dakika ya 66 akitumia vizuri pasi ya Kichuya, ambaye dakika 14 baadaye akapiga bao tamu la ushindi. Yanga bao lao walifunga dakika ya nne tu ya mchezo tena kwa penalti ya Simon Msuva.
Penalti yenyewe ilisababishwa na Novatus Lufunga yule ambaye alishindwa kumkaba Amissi Tambwe kwenye mechi ya kwanza aliyeipiga Simba bao la mkono. Jana akamwangusha Obrey Chirwa kwenye boksi, mashabiki walianza kummaindi kinoma, lakini baadaye wakamsamehe baada ya kupagawa na bao la Kichuya.
Hapo hapo, kumbuka Simba walikuwa kumi uwanjani baada yule beki Mkongomani aliyesajiliwa bure kupewa kadi nyekundu kwa kumkwida Chirwa nje kidogo ya boksi.
Kocha wa Simba, Joseph Omog, ni kama alibaki na mabao yake kwenye benchi kwani mabadiliko yake matatu aliyofanya ndiyo yaliyomaliza mchezo kiulaini kabisa.
Aliwaingiza Saidi Ndemla, Jonas Mkude na Kichuya. Wakatoka Lufunga, Mohamed Ibrahim na Juma Luizio. Hayo mabadiliko ndiyo yalichafua hewa Yanga wakapoteana katikati, watu wanamtafuta Haruna Niyonzima hawamuoni, wanamtafuta Mkata umeme hawamuoni. Mpaka Tambwe ambaye huwa anajipigiaga Simba kafichwa.
Yanga na makocha wake wote watatu ikalala 2-1. Yanga iliwatoa Mkata Umeme, Tambwe na Thabaan Kamusoko na kuwaingiza Deus Kaseke, Juma Mahadh na Said Makapu. Lakini haikusaidia kwani ikala kwao.
Kwa ushindi huo Simba imejikita zaidi kileleni ikiwa na pointi 54, tano mbele ya Yanga ambayo ni ya pili.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search