banner

February 27, 2017

KICHUYA ATOBOA YA UVUNGUNI

UMEMSIKIA winga wa Simba, Shiza Kichuya? Basi unaweza kusoma kwa umakini akichokizungumza baada ya kufunga bao la ushindi katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Yanga, uliochezwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika mchezo huo, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 2-1, lakini Kichuya alionekana ni shujaa zaidi baada ya kufanikiwa kuifungia Simba bao la ushindi, huku akiwa ndiye mtoa pasi ya bao la kusawazisha lililofungwa na Laudit Mavugo.
Kichuya alisajiliwa na Simba katika usajili mkubwa wa ligi hiyo, akitokea Mtibwa Sugar, ndani ya miezi mitatu aliisawazishia Simba dhidi ya Yanga  Oktoba mosi mwaka jana kwenye uwanja huo wa Taifa.
Juzi Kichuya alifunga bao muhimu kwa Simba dakika ya 81 na kuwafanya kuondoka na pointi tatu ambazo zimewaweka katika mazingira bora ya kutwaa ubingwa msimu huu.
Winga huyo amesema aligundua udhaifu wa mabeki wa Yanga ambao walikuwa wakichanganyana, hivyo alichoamua kila akipata mpira anauweka katikati ambapo kulikuwa na wenzake.
“Mwinyi hakuwa na mbio tena, maana kipindi cha kwanza alikimbia sana, nilipoona amechoka, niliamua kukatiza kwa kasi mbele yake na nilifanikiwa nikapiga krosi, ikazaa bao na mara ya pili nilipomtoka, nikaona nipige mwenyewe hasa kwa kuwa niliona kipa ameshatoka golini,” alisema.
Alisema alijua mechi ya Yanga ni ngumu na ilihitaji jitihada binafsi hasa kwa kuwa walikuwa nyuma, hivyo akaanza kujituma na akafanikiwa kutimiza lengo la kufunga bao na kusaidia bao la kusawazisha na kujiwekea krosi nzuri ya kuifunga Yanga akiwa na klabu ya Simba.
Katika hatua nyingine, Mavugo amesema licha ya ushindi huo, hawatabweteka kabisa kwa kuwa lengo hasa ni kutwaa ubingwa msimu huu.
“Ni mechi ngumu, lakini kuifunga Yanga si kwamba tumechukua ubingwa, tuna safari ndefu bado, hivyo naomba tusilewe na ushindi huu wa Yanga, tupambane hadi mwisho wa ligi kwa nguvu hii hii,” alisema.
Simba wanatarajia kucheza na Mbeya City, Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search