banner

February 25, 2017

REFA WAO

GOMA halilali leo. Ndiyo, hivyo ndivyo itakavyokuwa katika mchezo wa leo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao ni wa marudiano kati ya Simba na Yanga, utakaopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kuelekea pambano hilo, si Simba, si Yanga ambao wanatamani kupata sare zaidi ya kila upande kushuka dimbani ukiwa na dhamira moja tu, kupata ushindi.
Ni kutokana na hali hiyo, mchezo huo unatarajiwa kuwa na mchuano mkali kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho, kwani hakuna mchezaji atakayekubali kirahisi kutoka uwanjani kichwa chini.
Unajua kwanini imekuwa hivyo? Sababu zinaweza kuwa nyingi, lakini moja ndiyo inayoonekana kuwa na nguvu zaidi, si nyingine bali ni mbio za ubingwa wa ligi hiyo.
Kama ni utani wa jadi, huo umekuwapo kwa miaka lukuki. Kama ni heshima, tayari timu hizo zimeshatambiana mara kadhaa katika mechi za ligi hadi za michuano mingineyo.
Mchezo wa leo ni tofauti na mapambano mengine mengi ya watani hao, kwani umekuja wakati kukiwa na vita ya aina yake ya kuwania ubingwa baina ya wakongwe hao wa soka hapa nchini.
Katika msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom, Simba ipo kileleni ikiwa na pointi 51, baada ya kushuka dimbani mara 22, wakati Yanga waliocheza mechi 21 wakiwa nafasi ya pili na pointi zao 49.
Kutokana na hali hiyo, timu itakayoshinda leo ndiyo itakayokuwa na nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.
Unajua ni kwanini? Ni rahisi mno. Iwapo Simba watashinda watakuwa wamefikisha pointi 54, hivyo kuwaacha watani wao hao wa jadi kwa pointi tano, kiasi kwamba hata kama Yanga watashinda kiporo chao dhidi ya Mtibwa Sugar, watakuwa nyuma ya Wekundu wa Msimbazi kwa pointi mbili.
Ikumbukwe kuwa Yanga bado hawajarudiana na ‘wabishi’ Azam kiasi kwamba ni vigumu kuwa na uhakika wa asilimia 100 kushinda, tofauti na Simba ambao wamemaliza mechi zote dhidi ya timu ngumu.
Lakini pia hata kama Yanga wataifunga Azam, bado watateswa na pengo la pointi mbili, hivyo kujikuta wakiishia kuwafukuza Simba hadi mwisho ya ligi na hatimaye kushuhudia kombe likihama kutoka Mtaa wa Jangwani hadi ule wa Msimbazi.
Kwa upande mwingine, iwapo Yanga watashinda leo, watakuwa wamefikisha pointi 52 na hivyo kuwang’oa kileleni watani wao hao. Hali hiyo inaweza kuwapa faida kubwa Wanajangwani hao, kwani iwapo wataichapa Mtibwa katika mchezo wao wa kiporo, watafikisha pointi 55, hivyo hata kama watafungwa na Azam, bado watakuwa na nafasi kubwa ya kutetea ubingwa wao.
Kwa hali kama hiyo, kwanini mtanange wa leo uchache? Ni wazi kuwa hautachacha, timu mojawapo lazima ishinde. Zaidi ya hapo, ngoma ya ubingwa inaweza kuendelea kuwa mbichi.
Kwanini itakuwa mbichi? Kwa sababu iwapo timu hizo zitatoka sare, Yanga ikiichapa Mtibwa itafikisha pointi 53, hivyo kuiacha Simba kwa pointi moja tu na iwapo Wanajangwani hao wataangukia pua kwa Azam na watani wao kushinda mechi zao zote zilizobaki, kuna uwezekano mkubwa wa mwali kutua Mtaa wa Msimbazi.
Kuelekea mchezo wa leo, timu zote zimeonekana kujipanga vilivyo, ambapo Simba walikimbilia Zanzibar kusaka makali, huku Yanga wakijichimbia Kigamboni, Dar es Salaam.
Katika kuhakikisha ushindi unapatikana, klabu zote mbili zilihakikisha zinawadhibiti wachezaji wao kuepuka uwezekano wa kurubuniwa na wapinzani wao ili kuzihujumu timu, lakini pia makocha wakiwapa wachezaji wao mbinu na mikakati ya kutoka uwanjani vifua mbele.
Kwa upande wa vikosi, timu zote zimesheheni wachezaji wenye ubora wa kuwawezesha kutoa bonge la burudani kwa mashabiki, lakini pia ushindi kwa timu zao.
Mwisho wa siku, timu itakayokuwa makini, ikitumia vilivyo nafasi watakazozipata na kuepuka kufanya makosa, huku pia ikifanikiwa kuhimili presha ya mchezo, ndiyo itakayotoka uwanjani na ushindi.
Kikosi cha Simba, inayonolewa na Mcameroon Joseph Omog, kinatarajiwa kuundwa na wakali kama Daniel Agyei, Javier Bokungu, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Abdi Banda, Method Mwanjali, Jonas Mkude, Mzamir Yassin, James Kotei, Laudit Mavugo, Juma Luizio na Ibrahim Ajib.
Lakini pia, wapo Manyika Peter, Shiza Kichuya, Mohammed Ibrahim ‘Mo’, Hamad Juma, Novaty Lufunga, Mwinyi Kazimoto, Said Ndemla, Pastory Athanas na wengineo.
Kwa upande wa ‘Chama’ la Yanga chini ya kocha wake, George Lwandamina, watawategemea Deogratius Munish ‘Dida’, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Kelvin Yondani, Vincent Bossou, Jastin Zulu, Simon Msuva, Thaban Kamusoko, Amissi Tambwe, Obrey Chirwa na Haruna Niyonzima.
Wengine ni Ally Mustapha ‘Barthez’, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Oscar Joshua, Said Juma Makapu, Geoffrey Mwashiuya, Andrew Vincent ‘Dante’, Deus Kaseke, Matheo Anthony, Emmanuel Martin, Malimi Busungu na wengineo.
Tayari mwamuzi wa mchezo huo amefahamika baada ya kutangazwa jana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), mbaye ni Mathew Akrama kutoka Mwanza, huku wasaidizi wake wakiwa ni Mohamed Mkono (Tanga) na Hassan Zani (Arusha).

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search