banner

April 20, 2017

Mke wa Chameleon Adai Talaka Mahakamani Baada ya Kutishiwa Kifo

Mke wa Chameleon Adai Talaka Mahakamani Baada ya Kutishiwa Kifo

MKE wa mwanamuziki nguli nchini Uganda Joseph Mayanja maarufu ‘Jose Chameleone’ Daniella Atim amemtaka hakimu wa Mahakama ya mwanzo ya Nakawa kuivunja ndoa yao kutokana na ugomvi uliojitokeza baina yao.
Msanii huyo anadaiwa kumpiga na kumtukana pamoja na kuwatelekeza watoto wao wanne. Hati ya mashtaka namba 72 ya mwaka 2017, ilijazwa April 18, 2017 kwamba Chameleone alimnyanyasa yeye na watoto wake.
Kwa mujibu wa hati hiyo wawili hao walifunga ndoa Juni 7, 2008, katika kanisa la St. James Bbiina, Mutungo lililopo jijini Kampala na kubarikiwa kupata watoto wanne ndani ya ndoa.
Watoto hao ni Abba Mayanja, (11) Alfa Mayanja, (8) Alba Mayanja, (4) na Amama Mayanja, (3).
Kupitia kampuni ya Wanasheria ya Okurut, Atim alisema mwaka 2013 Chameleone alianza kumtesa na wakati mwingine alikuwa akirudi nyumbani amelewa na kumpiga bila sababu.
Ili kuficha maovu hayo na vidonda usoni Atim alikatazwa kwenda hospitali kupata matibabu na alikuwa akikimbilia nyumbani kwa marafiki zake ili kujificha.
Mwanamke huyo alisema kutokana na ukorofi wa Chameleone aliamua kumhama kitanda ili kujikinga na kuuliwa.
Atim alisema Chameleone hampi heshima mbele ya watoto kwa kumtukana mara kwa mara na wakati mwingine alikuwa akipiga na watoto pia.
“Maisha ya mlalamikaji yapo hatarini. Mtuhumiwa amekuwa akimtishia kumuua mara kwa mara na amemtesa sana,” ilisema taarifa ya hati hiyo.
Atim alisema mara kadhaa alijaribu kuwatafuta viongozi wa dini, ndugu na marafiki wa karibu wa mume wako ili kutafuta suluhu lakini Chameleone alikataa kila kitu.
Mwanamke huyo ameitaka mahakama kuivunja ndoa hiyo iliyodumu kwa miaka tisa na kutoa maamuzi ya moja kwa moja kuhusu suala hilo kumtaka Chameleone kulipa gharama zote za kesi hiyo.
Kesi hiyo imetajwa kwenye mahakama ya Mwanzo ya ya Margaret Aanyu. Chameleone amepewa siku 15 kwa ajili ya kujibu tuhuma hizo.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search