banner

April 22, 2017

SINAMTWA AFICHUA MADUDU SAKATA LA FAKHI

SINAMTWA AFICHUA MADUDU SAKATA LA FAKHI

WAKATI Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikitarajia kutoa uamuzi wake kesho kuhusiana na sakata la mchezaji, Mohamed Fakhi kudaiwa kucheza akiwa na kadi tatu za njano wakati wa mechi dhidi ya Simba, pia imefichua madudu iliyokutana nayo katika mahojiano na pande zinazohusika.
Kamati ya Saa 72 ya TFF iliipoka Kagera Sugar pointi tatu na mabao mawili ilizozipata katika mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Simba uliopigwa kwenye Uwanja wa Kaitaba ambapo wenyeji walishinda mabao 2-1.
Hata hivyo, uongozi wa Kagera Sugar uliandika barua TFF kuomba uamuzi huo wa kamati upitiwe upya kwa madai kwamba hawakutendewa haki.
Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji, Richard Sinamtwa, jana aliibuka na kusema kuwa ameshtushwa na sakata hilo akisema linaashiria mwenendo mbaya wa soka la Tanzania.
“Kazi ya kamati yangu ilikuwa kufanya mapitio ya kilichofanywa na Kamati ya saa 72, kuwapa pointi Simba kama ni sahihi na kama kilichofanyika kilikuwa ndani ya taratibu zao kama TFF.
“Pia Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji tuna mamlaka ya kusema kama Kamati ya saa 72 ilikosea na kutoa uamuzi upya au kuwaambia nini  wanatakiwa kufanya, lakini niseme bado tuna kazi ya kufanya kutafakari yote yaliyofanywa na kamati hiyo,” alisema Sinamtwa.
“Mpaka sasa zaidi ya asilimia 75 ya kazi imekamilika, bado 25, ila mpira wetu sijui unaenda katika hali gani, huwezi kupata watu watano wote wanaongea vitu tofauti na wote wabaki kuwa sawa.
“Kuna mazingara fulani ambayo ni lazima ufanye utafiti mpana. Taratibu zinatuelekeza kuwa ni taarifa gani tunapaswa kutumia.”
Katika hatua nyingine, uongozi wa klabu ya Simba umeliandikia barua Jeshi la Polisi kuomba maandamano ya amani kwa ajili ya kupeleka ujumbe wa malalamiko TFF kwani imekuwa ikifanya uonevu dhidi yao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa klabu hiyo, Haji Manara na kusainiwa na Rais wake, Evans Aveva, wameamua kuchukua uamuzi huo ili kuwasilisha kilio chao kwa Waziri wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,  Dk. Harrison Mwakyembe.
“Malalamiko mengi ya Simba yamekuwa yakisikilizwa kwa muda mrefu, pia  tumepata taarifa za TFF kumsimamisha Manara ili kumfunga mdomo asiweze kuongelea uovu uliopo katika Shirikisho hilo,” ilieleza taarifa hiyo.
Iliendelea kusema kuwa maandamano hayo yataanza saa 4. 00 asubuhi na makao makuu ya klabu ya Simba yakipitia barabara ya Msimbazi, Nyerere na Chang’ombe kuelekea Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kumwona waziri anayehusika.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search