banner

April 22, 2017

YANGA, PRISONS PATAMU LEO UWANJA WA TAIFA

YANGA, PRISONS PATAMU LEO UWANJA WA TAIFA

UTIMAMU na maandalizi mazuri ya saikolojia ndivyo vitu vinavyotarajiwa kuamua matokeo ya mechi ya Kombe la FA kati ya Yanga na Prisons itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mshindi wa mchezo huo ataungana na Simba, Mbao na Azam FC kucheza hatua ya nusu fainali ambapo bingwa ataiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho.
Ingawa inaonekana ni mechi nyepesi kwa Yanga kutokana na ubora wa kikosi chake kinachoundwa na wachezaji wenye majina, mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara bado watalazimika kuingia uwanjani kwa tahadhari kubwa kuikabili Prisons ambayo imedhamiria kupata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.
Kocha msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, akizungumzia maandalizi ya mchezo huo alisema anaamini kikosi chake kimeiva vya kutosha kupambana na Prisons na kupata ushindi.
“Kama unavyoona tunaendelea na mazoezi, vijana wapo fiti kwa ajili ya mchezo huo, tuna imani tutaibuka na ushindi kwa sababu kasoro zilizojitokeza  kwenye mechi za karibuni tumezirekebisha,” alisema.
Alisema matokeo waliyoyapata kwenye mchezo wao wa mwisho wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria, wameshayasahau na sasa wanapambana ili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo huo.
“Yale ya Alger tumeshayasahau ndio maana tunaendelea na maandalizi, Prisons wasitarajie mteremko kwa kuwa na sisi tumejipanga ipasavyo kuelekea mchezo huo,” alisema.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, akizungumzia mchezo huo aliwataka mashabiki wa timu hiyo waondoe shaka kwani lengo lao ni kuibuka mabingwa wa Ligi Kuu na Kombe la FA.
“Kwa kawaida katika soka timu inayojiandaa ndiyo inayoibuka na ushindi, kama wenzetu wanajiandaa sisi pia tunafanya hivyo, mashabiki waje uwanjani wapate burudani,” alisema.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search