banner

May 29, 2017

MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, POLE SIMBA SC

MALINZI ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI, POLE SIMBA SC

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi ametuma salamu rambirambi kwa Rais wa Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, Evans Aveva kutokana kifo cha shabiki wa timu hiyo, Shose Fedeline aliyefariki dunia, jana mchana Mei 28, 2017 katika ajali ya gari.
Kadhalika, Rais Malinzi ametuma salamu za pole kwa majeruhi katika ajali hiyo akiwamo nahodha wa Simba, Jonas Mkude na dereva wa gari hilo ambalo lilikuwa safarini kurejea Dar es Salaam kutoka Dodoma.
Wanafamilia kadhaa wa mpira wa miguu walikuwa Dodoma mwishoni mwa wiki iliyopita kushuhudia mchezo wa fainali za Kombe la Azam - ASFC (Azam Sports Federation Cup HD 2016/17) uliozikutanisha timu za Simba na Mbao FC ya Mwanza. Mbao ilifungwa mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa dakika 120.
Gari lililopata ajali ni aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilianguka na kuzunguka mara kadhaa na baadaye kutulia katika eneo la Dumila mkoani Morogoro baada ya tairi yake ya nyuma kupasuka hivyo kumshinda dereva na kupoteza mwelekeo kutoka barabara kuu.
“Nakuandikia Rais wa Simba, Bw. Evans Aveva, pia ndugu, jamaa na marafiki pamoja na majirani wa marehemu Shose Fideline na wanafamilia wengine wa mpira wa miguu, kwamba nimepokea taarifa za ajali ya gari iliyosababisha kifo cha mmoja wa mashabiki wa timu ya Simba kwa masikitiko makubwa sana. Wito wangu, nawaomba wanafamilia wote kuwa watulivu na moyo wa subira katika kipindi hiki kigumu,” amesema Rais Malinzi.
Msiba wa shabiki huyo wa Simba umetokea wakati Simba imetawazwa kuwa mabingwa wapya wa Kombe la Azam likihitimisha ushindani wa timu 86 na hivyo kuwa na hati ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika (CAF) hapo mwakani.
Mwenyezi Mungu ampe mapumziko mema, Shabiki wa Simba, Shose Fedeline.
“Pia nawapa pole nyingi sana majeruhi wote katika ajali hiyo akiwamo Jonas Mkude ambaye ni Nahodha wa Simba na Nahodha Msaidizi wa Timu ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Nawaombea kwa Mwenyezi Mungu majeruhi wote wapone haraka ili kujiunga na shughuli zao mbalimbali za ujenzi wa nchi,” amesema Rais Malinzi.
Kadhalika, Rais Malinzi ameipongeza Simba kwa kutwaa ubingwa huo wa ASFC hivyo pamoja na zawadi nyingine kama vile Sh 50 milioni na medali za ubingwa pia Simba imepata tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Shirikisho - michuano inayoandaliwa na CAF.
“Naitakia Simba maandalizi mema ya kushiriki michuano ya kimataifa hapo mwakani,” amesema Rais Malinzi.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search