banner

June 20, 2017

AJIB, GADIEL WAMTIA ‘KIBRI’ SINGANO

AJIB, GADIEL WAMTIA ‘KIBRI’ SINGANO

SALMA MPELI NA MSAFIRI ULIMALI, (DSJ)
HUENDA idadi ya wachezaji wa Azam FC kuihama timu yao, ikazidi kuongezeka baada ya winga wao, Ramadhan Singano, waliyemsajili kutoka Simba, kuhusishwa na taarifa hizo.
Mkataba baina ya Singano na Azam unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu ambapo hadi sasa ameshindwa kufikia mwafaka na viongozi wake kwa ajili ya mkataba mpya.
Taarifa kutoka Azam FC zinadai kuwa pande hizo mbili zimeshindwa kuafikiana kutokana na Singano kudaiwa kutaka dau kubwa ambalo uongozi unaonekana kutokuwa radhi kutoa.
Singano ambaye ni mmoja wa wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kutumia mguu wa kushoto, anatajwa kutakiwa na Yanga na huenda taarifa za wenzake, Ibrahim Ajibu wa Simba na Daniel Michael wa Azam kusemekana wamesajiliwa na dau kubwa, zikawa zinampa kiwewe naye akitaka kuondoka ili kufaidi matunda hayo.
Baada ya taarifa hizo kuenea mitaani, BINGWA lilizungumza na Singano ili kupata ukweli wa jambo hilo ambapo alionekana kushikwa na kigugumizi huku akidai ataweka wazi kila kitu baada ya kumalizika kwa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Siwezi kuzungumzia chochote kwa sasa juu ya mustakabali wangu na Azam wala hayo masuala ya Yanga, nipo kwenye mfungo na utakapomalizika kila kitu kitakuwa wazi,” alisema winga huyo.
Mpaka sasa Azam FC imeondokewa na wachezaji wake watatu muhimu ambao ni John Bocco, Aishi Manula pamoja na Shomari Kapombe waliojiunga na Simba, huku beki wa kushoto, Gadiel Michael akitajwa kumalizana na Yanga.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search