banner

October 11, 2019

MTIBWA SUGAR KUJENGA UWANJA WA KISASA, WAILILIA TFF

MTIBWA SUGAR KUJENGA UWANJA WA KISASA, WAILILIA TFF


Uongozi wa klabu ya Mtibwa Sugar umeanza mchakato kujenga kiwanja chake kitakachokuwa na uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 20,000 mjini Manungu, Morogoro.

Mtibwa wameamua kuanza harakati za kujenga uwanja wao baada ya kiwanja cha Manungu ambacho hukitumia kwa mechi za mashindano yao yote kufungiwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF).

Ofisa Habari wa Mtibwa, Thobias Kifaru, amesema tayari wakandarasi wameshapatikana na wataanza kuandaa ramani ya uwanja huo wiki hii.

Licha ya kuchukua kuchukua zaidi ya watu elfu ishirini, Kifaru ameeleza uwanja huo utajengwa umbari wa kilomita mbili kutoka karibu kwenye makazi ya watu ili kuwapa urahisi wa kufika wakati timu hiyo ikicheza.

"Baada ya TFF kufungia uwanja wetu, tumeona ni vema tukajenga uwanja ambao utakuwa na hadhi na wa kisasa zaidi.

"Tumefanya maamuzi haya sababu hatuutumii tena uwanja wa Manungu na badala yake tumepelekwa Jamhuri Morogoro, kitu ambacho kimetufanya tutumie gharama ambazo ni kubwa kwetu, imekuwa kama tunaenda kucheza ugenini vile.

"Tumekuwa tunatumia takribani zaidi ya milioni tano tukienda Jamhuri, hii ni kutokana na gharama za kula, kulala na hata mafuta ya gari.

"Uwanja wetu utakuwa umbali wa kilomita mbili kutoka eneo la makazi ya watu na wahusika watakaochora ramani wataanza kazi hiyo wiki hii," amesema Kifaru.

Kwa upande mwingine, Kifaru amefunguka kuwa, wao kama Mtibwa wametuma barua TFF kuomba waendelee kutumia uwanja wa Manungu kwa msimu huu kutokana na gharama za kwenda Jamhuri Stadium kuwa kubwa.

Ameeleza "ni vema TFF wakatuangalia kwa namna timu yetu ambavyo imekuwa ikitoa mchango ndani ya taifa hili ikiwemo vijana wetu waliopo Ngorongoro Heroes, watuachie tutumie Manungu kuliko kwenda Jamhuri ambako tunatumia kiasi kikubwa cha pesa."




Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search