banner

June 22, 2021

KIPA METACHA MNATA ALICHEZA YANGA BILA KULIPWA

KIPA METACHA MNATA ALICHEZA YANGA BILA KULIPWA


 HIVI sasa kipa wa Yanga, Metacha Metacha hayupo kwenye kikosi hicho baada ya kusimamishwa kutokana na kuonyesha ishara isiyofaa kwa mashabiki wakati timu yake ikiwashinda Ruvu Shooting 3-2, kwenye Uwanja wa Mkapa.

 

Metacha alionyesha ishara ya kidole chenye tafsiri mbaya kwa mashabiki, baada ya kuzomewa kwa madai kuwa alicheza chini ya kiwango na kupelekea kufungwa mabao ambayo mashabiki walitafsiri kama uzembe.

 

Wakati Metacha akikumbwa na kadhia hiyo mengi yanasemwa ikiwemo kuhusishwa kwenda Simba na mashabiki wakidhani kuwa hiyo ndiyo sababu ya kipa huyo kuruhusu mabao ya makusudi na kwamba haipendi klabu hiyo kwa sasa.

 

Sasa meneja wa kipa huyo, Jemedari Said amefunguka mambo mapya akidai kuwa siyo kwamba mteja wake huyo haipendi klabu hiyo kwani ingekuwa hivyo angeshaondoka tangu zamani kwa kuwa mpaka sasa hajamaliziwa fedha yake ya usajili.

 

Mbali na hilo Jemedari alikwenda mbali zaidi akisema Metacha alicheza nusu ya msimu akiwa hajalipwa hata fedha kidogo na bado aliipambania timu.

 

“Siyo kweli kuwa Metacha amefanya makosa ya kinidhamu kwa sababu haipendi Yanga na anataka kuondoka.


“Kwani hadi sasa bado anawadai hela yake ya mwaka jana, mbali na hivyo alicheza nusu msimu akiwa hajalipwa fedha yoyote, hivyo hiki kinachotokea sasa hakihusiani kabisa na ishu za yeye kutajwa kuondoka Yanga.

 

KUHUSU KUFUNGIWA NA YANGA

“Yanga wamefanya jambo nzuri sana kuchukua maamuzi mapema, kwa sababu baada ya mechi mimi nilizungumza na Metacha na nikamwambia wazi kuwa sijapenda alichokifanya na siyo kitendo cha kiungwana.

 

“Na nikamwambia wazi kuwa akae tayari kwa lolote kutoka Yanga, kwa sababu hawatoweza kuvumilia kwa kuwa mimi naifahamu Yanga tofauti na watu wanavyofikiria na kwa bahati nzuri Yanga wakachukua hatua,” alisema Jemedari.


Chanzo: Championi



Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search