banner

April 19, 2024

BENCHIKA AMUACHIA MATOLA MKUTANO NA GAMONDI KABLA YA MECHI YA WATANI KESHO

BENCHIKA AMUACHIA MATOLA MKUTANO NA GAMONDI KABLA YA MECHI YA WATANI KESHO


KOCHA Mkuu wa Simba SC, Abdelhak Benchika amewakilishwa na Msaidizi wake, Suleiman Matola kwenye mkutano na Waandishi wa Habari, wakati Kocha Mkuu wa Yanga, Muargntina Miguel Angel Gamondi amefika mwenyewe kuelekea mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania.
Simba atakuwa mgeni wa Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu kesho kuanzia Saa 11:00 jioni Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam na leo asubuhi umefanyika Mkutano na Waandishi wa Habari ambao huhusisha Makocha na Manahodha wa timu.
Gamondi amefika mwenyewe na kusema kwamba utakuwa mchezo mgumu, kwani wapinzani wao watakuja kucheza kwa lengo la kushinda ili walipa kisasi cha kufungwa 5-1 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza Novemba 5 mwaka jana.
"Lakini tumejiandaa kwa hilo, sisi tuna timu imara ambayo inaweza kucheza kwenye presha ya aina yoyote. Kama wanadhani wakija na presha ya kulipa kisasi inaweza kuwasaidia basi linaweza pia kuwa kosa," amesema Gamondi.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi wa Simba SC Suleiman Matola amesema kwamba wataingia kwenye mchezo wa kesho wakiwa na mbinu tofauti na walizotumia kwenye mechi ya Novemba 5 wakichapwa 5-1 hapo hapo Benjamin Mkapa.
"Tunakwenda katika mchezo huu tukiwa na mbinu tofauti na michezo iliyopita, kwani mechi hii si ya kuangalia rekodi ya timu gani ilifanya jambo gani nyuma, bali kila kitu kinakuwa kipya," amesema Matola.  
Timu zote mbili ziliwakilishwa na wachezaji ambao si Manahodha, mbeki Dickson Job upandewa Yanga na Shomari Kapombe kwa Simba SC.
"Simba SC ni timu nzuri, nasi tuna timu nzuri, bila shaka utakuwa mchezo mzuri wenye ushindani hivyo tumejiandaa vyema sana kuhakikisha tunaondoka na alama tatu muhimu," amesema Job.
"Tumefanya maandalizi mazuri na benchi la Ufundi limekuwa likifanya masahihisho kwenye mapungufu na kuongeza uimara kwenye maeneo tuliyokuwa bora. Wachezaji wote tupo tayari kwa ajili ya mchezo wa kesho ili kupata ushindi,"amesema Kapombe.


source http://www.binzubeiry.co.tz/2024/04/benchika-amuachia-matola-mkutano-na.html

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search