banner

February 26, 2017

HABARI KUBWA 6 ZA MICHEZO NA TETESI ZA USAJILI ULAYA FEBRUARI 26

HABARI KUBWA 6 ZA MICHEZO NA TETESI ZA USAJILI ULAYA FEBRUARI 26

UNITED KUMFUNGIA KAZI NEYMAR
Taarifa kutoka nchini Uingereza zinasema kuwa meneja wa Manchester United Jose Mourinho amekuwa akimpigia simu Neymar na kumtaka ajiunge na Mashetani Wekundu hao.
Neymar amesaini mkataba mpya mwaka jana ambao utailazimu United kutoa dau lisilopungua Euro 200 milioni ili kupata saini ya nyota huyo.
Neymar amekuwa kwenye kiwango bora tangu atue Barcelona akitokea Santos ya Brazil kwa ada ya uhamisho ya paundi 57 milioni ingawa kulikuwa na misukosuko juu ya ada halisi ya uhamisho wake.
DORTMUND YAIFARIJI LIVERPOOL

Mkurugenzi wa klabu ya Borussia Dortmund Hans-Joachim Watzke ametoa maneno ya kuifariji klabu ya Liverpool katika mipango yao ya kumsajili winga wao Christian Pulisic.
Purisic 18 amekuwa katika orodha ya vijana hodari wanaochipukia katika soka la Ujerumani na kuwafanya Majogoo hao wa Anfield kuhitaji huduma za kinda huyo.
“Katika idara ya ushambuliaji tuna watu wengi na tunahtaji kupunguza wengine” kauli hii ya Watzke huenda ikawavutia Liverpool kuandaa dau.
IBRAHIMOVIC KUIKACHA UNITED

Mshambuliaji hatari wa Manchester United Zlatan Ibrahimovic hana uhakika kama atasaini mkataba mpya klabuni hapo kutokana na kuhitaji kucheza ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo Mashetani hao wanaweza wakashindwa kushiriki.
Ibrahimovic alijiunga na United akitokea PSG ambayo imekuwa ikishiriki mara kwa mara Klabu bingwa barani Ulaya kitu ambacho kimekuwa kigumu kwa vijana hao wa Old Trafford katika siku za karibuni.
United wapo nafasi ya sita katika msimamo wa ligi kuu nchini Uingereza na huenda wakakosa tena nafasi ya kushiriki michuano na kusababisha raia huyo wa Sweden kutimka klabuni hapo.
CHELSEA WAMTAKA CASEMIRO

Kiungo Mbrazil Carlos Henrique maarufu kwa jina la ‘Casemiro’ amekuwa katika orodha ya nyota wanaohitajiwa na klabu ya Chelsea.
Casemiro ambaye kwasasa ni kiungo tegemeo katika klabu ya Real Madrid chini ya kocha Zinedine Zidane ameivutia klabu ya Chelsea kutokana na uwezo wake wa ‘kukata umeme’ awapo dimbani.
Mbali na Chelsea klabu ya Manchester United pia imeonyesha nia ya kumuhitaji Mbrazil huyo ambaye alifanya kazi na kocha Jose Mourinho kipindi cha mwisho cha Mreno huyo akiwa Madrid.
LUKAKU AFIKIA REKODI UFUNGAJI MUDA WOTE EVERTON

Mshambuliaji wa Everton Romelu Lukaku amefikia rekodi ya ufungaji wa muda wote wa klabu hiyo iliyokuwa ikishikiliwa na Duncan Ferguson.
Lukaku amefikia rekodi hiyo baada ya kupachika bao la pili na la ushindi katika mechi dhidi ya Sunderland katika dimba la Goodison Park waliposhinda mabao 2-0. Rekodi hiyo ya Ferguson ilidumu tangu msimu wa 2005-06 baada ya kustaafu.
Mshambuliaji huyo ameendelea kuwa na msimu mzuri klabuni hapo na huenda akavuka idadi ya mabao 18 katika ligi kuu aliyopachika msimu uliopita akiwa na mabao 17 mpaka sasa huku kukiwa na mechi kadhaa kabla ya ligi hiyo kumalizika.
NEUR ACHEZA MICHEZO 100 BILA KUFUNGWA BUNDESLIGA

Mlinda mlango wa Bayern Munich Manuel Nuer amefikisha michezo 100 bila kufungwa katika ligi kuu nchini Ujerumani ‘Bundesliga’ katika ushindi wa mabao 8-0 dhidi ya Hamburg SV.
Katika mechi hiyo ambayo ilikuwa ni ya muhimu kwa Carlo Ancelotti aliyefikisha mchezo wa 1000 akiwa kocha ilishuhudiwa wenyeji hao wakitoka kifua mbele huku mlinda mlango huyo nyavu zake zikiwa hazijatikiswa.
Kipa huyo amefikisha michezo 100 bila kufungwa kati ya mechi 183 alizochezea timu hiyo huku akiwa ni tofauti wa michezo 49 na golikipa yoyote yule katika historia ya ligi hiyo.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search