SERIKALI inatarajia kupiga marufuku utengenezaji na uingizaji wa pombe
za bei rahisi maarufu kama `Viroba' nchini ndani ya miezi mitatu ijayo
sawa na siku 90.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk.
Hamisi Kigwangalla, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma juzi alipokuwa
akijibu hoja za wabunge waliokuwa wakilalamikia kilevi hicho kutokana na
kupunguza nguvu kazi ya Taifa wakati wa uwasilishwaji wa taarifa za
Kamati ya Bunge ya Masuala ya Ukimwi na ya Huduma na Maendeleo ya Jamii
kwa mwaka 2016/17.
Dk. Kigwangalla alisema kuwa baada ya miezi mitatu, kilevi hicho
kitapigwa marufuku kutengenezwa au kuingizwa nchini pamoja na kuziba
mianya yote ya uingizaji.
Alisema kilevi hicho hutumiwa na vijana wengi na hivyo kuharibu nguvu kazi ya Taifa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini Esther Matiko, amesema
kwamba pombe hiyo inasababisha vifo vya vijana wengi nchini ambao ndio
tegemeo kubwa na nguvu kazi ya Taifa.
“Katika kipindi hiki kifupi cha likizo yangu, nilikuwa jimboni kwangu na
tumezika vijana wanne waliofariki dunia kutokana na matumizi ya viroba.
Hivyo wananchi wa jimbo langu wameniagiza kuja kulieleza Bunge athari za
pombe hiyo ili tujadili na kuona namna gani ya kuliokoa Taifa hasa
vijana kutoka katika janga hilo,” alifafanua Matiko.
Akiwasilisha taarifa ya Kamati, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dk. Faustine
Ndugulile, alisema kuwa Kamati imebaini uwepo wa uhusiano mkubwa kati ya
matumizi ya pombe hizo na kuongezeka kwa tabia hatarishi zinazochangia
ongezeko la vijana katika matumizi ya dawa za kulevya.
Aidha, alisema hali hiyo inaathiri ufanisi wa nguvu kazi ya Taifa kutokana na madhara ya matumizi ya dawa za kulevya.
Post a Comment