banner

February 24, 2017

WEMA SEPETU AHUDHULIA KESI YA MBOWE

WEMA SEPETU AHUDHULIA KESI YA MBOWE

MSANII nyota wa filamu nchini, Wema Sepetu amehudhuria kesi ya Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe.
Wema ambaye pia aliwahi kuwa Miss Tanzania mwaka 2006, alikuwa na mama yake katika kesi hiyo, akiwa amekaa pamoja na Mbowe na viongozi wengine wa Chadema wakiwamo wabunge. Imeelezwa kuwa mrembo huyo amejiunga na chama hicho baada ya kukimbia Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Katika taarifa ya Ofisa Habari wa chama hicho, Emmanuel Makene jana alisema Mbowe angezungumza na umma kupitia waandishi wa habari kukaribisha wanachama wapya waliojiunga jana akiwemo Wema.
Hata hivyo, nje ya mahakama, Lissu alisema wamefika hapo kwa ajili ya kesi hiyo ya mwenyekiti wao na hilo la wanachama wapya halitazungumzwa kwa wakati huo.
Ndani ya mahakama, hata hivyo, jopo la Wanasheria wa Serikali likiongozwa na Gabriel Malata, Paul Shaidi na Sylvester Mwakitalu, ulitoa mapingamizi kupinga maombi ya mdai yasikubaliwe mahakamani kwamba yanamakosa kisheria na yameletwa nje ya muda.
Katika Kesi hiyo ya kikatiba Namba 1 ya mwaka 2017, Mbowe anapinga mamlaka ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda hiyo, Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa kanda hiyo (ZCO) Camilius Wambura, ya kutaka kumkamata hadi maombi hayo yatakaposikilizwa. Aidha, Polisi wanaweza kumuita Mbowe kwa ajili ya mahojiano na kuendelea na upelelezi pindi watakapomuhitaji.
Maombi hayo yalianza kusikilizwa kuanzia saa 8 mchana hadi saa 12 jioni mbele ya jopo la majaji watatu likiongozwa na Sekieti Kihiyo, akisaidiana na Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Pellagia Kaday huku upande wa mdai ukiwa na Wanasheria Tundu Lissu na Peter Kibatala.
Akiwasilisha mapingamizi yao, Malata alidai kuwa maombi hayo yameletwa chini ya sheria isiyotakiwa na kwamba hayana mashiko. Malata alidai maombi hayo yameletwa nje ya muda kwa kuwa tayari Mbowe alikamatwa, alifanyiwa mahojiano na aliachiwa na Polisi.
‘’Hati ya kiapo cha mdai (Mbowe) ina mapungufu kwa sababu kwa mujibu wa sheria kiapo kinatakiwa kielezee facts (maelezo) na sio mawazo ya mtu hivyo sio sahihi tunaomba maombi haya yatupiliwe mbali kwa gharama ya kesi,’’ alidai Malata.
Pia alidai kuwa kiapo hicho ndio kinabeba maombi ya mdai hivyo yakiwa na mapungufu hata maombi yake yanakuwa na mapungufu.
Malata alidai maombi hayo yanahusiana na kesi za jinai na kwamba Mahakama Kuu haina mamlaka ya kutoa maamuzi yanayohusiana na jinai hivyo, wadai walipaswa kupeleka kesi hiyo katika mahakama husika.
Akijibu mapingamizi hayo, Wakili Kibatala alidai kuwa mwanasheria wa serikali alitakiwa kuonesha ni kifungu gani cha sheria ambacho kingeiongoza mahakama katika njia sahihi kuhusu maombi hayo.
Pia alidai kuwa sheria iliyotumika kufungulia maombi hayo iko sahihi hivyo kungekuwa na mapungufu upande wa wadaiwa ungeonesha ni sheria ipi.
Hata hivyo, katika hoja ya kuingizwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) katika kesi hiyo liliibuliwa lakini mahakama iliamuru upande wa wadai urekebisha maombi yao kwa kuwa hawakumuingiza Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) licha ya kuishitaki serikali.
“Tutafanya marekebisho ya maombi yetu na marekebisho mengine madogo madogo kwa namna tutakavyoona inafaa siku ya jumatatu na tutawapa wajibu maombi Machi 6, mwaka huu na Machi 8, mwaka huu itatajwa kwa ajili ya kusikiliza maombi hayo,” alidai Lissu.
Katika kesi ya msingi, Mbowe anaomba mahakama iwazuie wadaiwa kutekeleza azma yake ya kumtia mbaroni pia itoe amri ya kuwazuia kumkamata hadi hapo kesi hiyo ya kikatiba itakapomalizika na kwamba polisi wasiendelee na mchakato wowote dhidi yake hadi hapo kesi hiyo itakapomalizika.
Anadai kuwa sheria inayompa Mkuu wa Mkoa mamlaka ya kutoa amri ya kumkamata na kumweka ndani mtu iko kinyume cha katiba, kwa madai kuwa ilitungwa katika mazingira ambayo hapakuwa na vituo vya polisi vya kutosha. Pia anadai kuwa kwa mazingira ya sasa sheria hiyo imeshapitwa na wakati na anaiomba mahakama itamke kuwa ni kinyume cha katiba.
Mbowe pia anadai kuwa hata kama Mkuu wa Mkoa alikuwa anatekeleza mamlaka yake kwa mujibu wa sheria hiyo basi hakutimiza matakwa ya kisheria, ambayo ni pamoja na kutoa taarifa kwa Hakimu wa Mahakama ya Wilaya au ya Hakimu Mkazi.
Vile vile, anaiomba mahakama kama itaona kuwa Mkuu wa Mkoa alikuwa sawa kutoa amri hiyo basi imwamuru afuate matakwa ya kisheria, ikiwa ni pamoja na kulinda haki za binadamu katika kutekeleza madaraka yake hayo. Maamuzi ya mapingamizi hayo yatatolewa Machi 2, mwaka huu.

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search