banner

April 10, 2017

LAMPARD : NILIKATAA KUFANYA KAZI NA MOURINHO

LAMPARD : NILIKATAA KUFANYA KAZI NA MOURINHO

Aliyekua kiungo wa timu ya taifa ya England Frank Lampard amefichua siri kuhusu msimamo wa kuzikataa ofa za klabu nguli nchini Hispania Real Madrid, Barcelona pamoja na Inter Milan ya Italia.
Lampard ambaye aliitumikia Chelsea kwa kipindi cha miaka 13 amepasua siri hiyo, baada ya kuhojiwa na gazeti la The Sun ambalo lilitaka kufahamu taarifa hizo, ambazo ziliwahi kusikika kama tetesi miaka ya nyuma.
Lampard, mwenye umri wa miaka 38, amesema ni kweli klabu hizo ziliwahi kutuma ofa ili zimsajili kwa nyakati tofauti, lakini aliweka msimamo wa kubaki Stamford Bridge.
Amesema lengo lake lilikua ni kutaka kucheza soka kwa kipindi kirefu akiwa na klabu moja na lengo hilo lilitimia akiwa na The Blues kabla ya kutimkia nchini Marekani mwaka 2014.
“Siku za nyuma niliwahi kukataa ofa za klabu hizi, na kwa bahati nzuri ofa hizi zilikuja wakati Jose Mourino akiwa kwenye benchi la ufundi la Real Madrid na Inter Milan.
“Sikutaka kabisa kuitikia wito wa klabu hizo, nilielekeza nguvu na mapenzi yangu Chelsea na nilitamani kucheza katika maisha yangu yote nikiwa magharibi mwa London, na kwa asilimia kubwa nilifanikiwa.
“Niliamini kwenda katika moja ya klabu hizi tatu, ingenichukua kipindi kirefu kuzoea mazingira ambayo yangekua mageni kwangu, hivyo sikutaka kabisa hilo litokee katika maisha yangu ya soka.” Alisema Lampard
Lampard alianza kuitumikia Chelsea mwaka 2001 na aliondoka klabuni hapo mwaka 2014 kuelekea nchini Marekani, ambapo alisajiliwa na klabu ya New York City inayoshiriki ligi ya MLS.
Hata hivyo Lamprad alirudi nchini England akiwa na Man city baada ya kusajiliwa kwa mkopo akitokea Marekani, na kisha alirejea na kucheza hadi mwezi August mwaka 2016 baada ya mkataba wake kufikia kikomo.
Klabu nyingine ambazo Lampard aliwahi kuzitumikia ni West Ham Utd na Swansea City.

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search