banner

May 26, 2019

WANNE WA KIMATAIFA WATUA YANGA

WANNE WA KIMATAIFA WATUA YANGA


KOCHA Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewaonyesha rasmi viongozi wachezaji aliomalizana nao wakapagawa kwa furaha. Zahera amewaambia kwamba atasajili wachezaji sita wa kigeni, lakini amewaonyesha wanne ambao ni beki, viungo wawili na straika na ameshamalizana nao kabisa na akawasisitiza kuwa hawa ni mali ya Yanga kabisa.

Wachezaji hao ambao watatua Dar es Salaam muda wowote kuanzia wiki ijayo ni kiungo Alex Komenan, beki wa kati Mohammed Camara (Guinea), Victor Patrick Akpan ambaye ni kiungo mkabaji na straika Shehu Magaji Bulama ambaye Zahera amewasisitiza vigogo hao kwamba ni zaidi ya Heritier Makambo aliyetimkia Horoya ya Guinea.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema Zahera amewaambia viongozi kwa kikao chao kwamba wachezaji hao wote wanatokea kwenye nchi zinazozungumza Kifaransa na anawajua vilivyo wala hana wasiwasi nao na wote ni huru kwa sasa.

Habari zinasema kwamba mkongomani huyo mwenye uraia wa Ufaransa amewaambia vigogo hao kwamba yuko kwenye hatua za mwisho za kumalizana na kipa wa Bandari ya Mombasa, Farouk Shikalo. Kocha huyo amepanga kuwatangaza wachezaji hao wote Jumanne ijayo jioni baada ya mechi na Azam FC kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Habari ambazo Championi Jumamosi imejiridhisha nazo ni kwamba Zahera amewahakikishia viongozi kwamba wachezaji hao wameshasaini mikataba ya awali ya miaka miwili na amewaonyesha kwenye WhatsApp yake wakachekelea.

Aliwasisitiza kwamba anataka kutengeneza Yanga babkubwa ambayo itarejesha hadhi ya klabu ndio maana ameamua kuchukua watu wa kazi tena kwa gharama rafiki kwa klabu tofauti na longolongo za miaka ya nyuma. “Ana listi ya wachezaji wengi lakini anataka sita tu wa kigeni.

Tayari amemalizana na wanne ambao ni Komenan (kiungo mchezeshaji), Camara (beki wa kati), Akpan (kiungo mkabaji) na Bulama yeye ni mshambuliaji anayekuja kuchukua nafasi ya Makambo.

“Hao ni kutoka nje ya nchi, pia wapo wawili ambao nao atawatangaza hivi karibuni mara baada ya mchezo wa ligi wa mwisho kumalizika dhidi ya Azam FC,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Zahera kuzungumzia hilo alisema kuwa: “Mikakati ya usajili inakwenda vizuri na nimepanga kusajili wachezaji nane pekee na kati ya hao sita wa kimataifa na hao wengine wawili wazawa.

“Na nilishatangaza kuwa kati ya hao yupo mshambuliaji mmoja kutoka Guinea na hao wengine nitawangaza mara baada ya mechi ya ligi na Azam Mei 28 ya wiki ijayo baada ya mchezo huo, pia na wale nitakaowaacha,” alisema Zahera.

Habari zinasema baada ya mechi na Azam pia atatangaza listi yote ya wachezaji anaowatema na wanaosalia Yanga siku ya kuanza kambi ya maandalizi. Kocha huyo amekamilisha zoezi hilo la usajili mapema kabla ya wiki ijayo kuondoka kwenye Hispania kujiunga na DR Congo inayojiandaa na Afcon.

CHANZO: CHAMPIONI

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search