banner

October 13, 2019

SIFIKIRII KUSOTA KWA NDEMLA BENCHI NDANI YA SIMBA ILA NAFIKIRIA UWEZO WA KWENYE MGUU UNAVYOYEYUKA

SIFIKIRII KUSOTA KWA NDEMLA BENCHI NDANI YA SIMBA ILA NAFIKIRIA UWEZO WA KWENYE MGUU UNAVYOYEYUKA


SAID Ndemla ni mchezaji nyota ndani ya klabu ya Simba ambaye jina lake kwa sasa si miongoni mwa yale yanayotamkwa sana kutokana na kutokuwa na nafasi ya kudumu ndani ya kikosi cha Simba.

Mwanzoni Ndemla alikuwa anapata nafasi kikosi cha kwanza ila haikuwa wakati wa Kocha Mkuu Patrick Aussems hii inatokana na mifumo ambayo anaitumia kocha huyo pamoja na mbinu zake.

Achana na mbinu za kocha huyu, bado kuna kitu ambacho kipo kwenye miguu ya Ndemla kama hatashtuka wakati utamuacha na mguu wake utamkataa.

Ukimtazama kwa haraka, Ndemla ni mchezaji ambaye amekata tamaa kutokana na kutojipa nafasi ndani ya Simba kwani mwenyewe aliwahi kukiri kuwa ni ngumu kwake kupata namba ndani ya Simba.

Kwa nini aliamua kusema hivyo, alitazama aina ya wachezaji waliopo ndani ya Simba na akasahau kwamba hao wote waliokuja kwa sasa ndani ya Simba wamemkuta akiwa ni nyota.

Achana na suala la kumkuta ndani ya Simba nazungumzia kipaji halisi ambacho kinaishi kwa muda kwenye miguu ya Ndemla.

Hana papara akiwa ndani ya uwanja kila anachokifanya licha ya kuwa ni kiungo anafikiria kuipa ushindi timu yake.

Mtazame kwenye mechi ambazo amepata nafasi ya kucheza katika mipira mitatu atakayopiga mmoja ni lazima ulenge kwenye lango na anakuwa na hatari wakati hakuna anayemfikiria.

Akiwa nje ya 18 ndipo mguu wake na uwezo wake wa mguu wa kulia unaonekana lakini bado hajazinduka anakubali kuacha uwezo wake kwenye mguu unayeyuka taratibu.

Mkumbuke yule Ndemla aliyecheza na KMC msimu uliopita, mtazame namna alivyomalizia pasi ya Mzamiru Yassin alikuwa nje ya 18 na kwa utulivu kabisa alifanya kweli.

Ndemla kwa sasa unakwama wapi? Ni nani aliyekushikia mguu wako, ni wakati wa kuzinduka na kutafuta namna ya kuufufua uwezo wako mguuni mwako.

Lile tabasamu lako linalotokana na mashuti yako ya mbali inabidi ulirudishe, rudisha hali ya kujiamini na ufanye vizuri zaidi ya jana.

Bado sijapata muda wa kufikiria kuhusu kukaa kwako benchi ndani ya Simba ila nafikiria uwezo wako unavyoyeyuka kwenye mguu wako.


Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search