banner

March 24, 2024

MSEMAJI WA SERIKALI MATINYI AFAFANUA KAULI YA WAZIRI NDUMBARO MECHI ZA SIMBA NA YANGA

MSEMAJI WA SERIKALI MATINYI AFAFANUA KAULI YA WAZIRI NDUMBARO MECHI ZA SIMBA NA YANGA


MKURUGENZI wa Idara ya Habari, MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ametoa ufafanuzi kuhusu kauli ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro kwamba Shabiki atakayekwenda uwanjani kutazama mechi za Kimataifa za Simba na Yanga anapaswa kuvaa jezi za Simba au Yanga, kinyume na hapo atalazimika kuwa  na Hati ya kusafiria  ya Nchi ambayo klabu anayoishangilia inatokea au vinginevyo hatoruhusiwa kuingia uwanjani.
Msemaji Mkuu katika ufafanuzi wake leo Machi 24, 2024 katika Mkutano wake na Vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam amesema Waziri alikuwa anahamasisha  uzalendo wa timu na hakumaanisha kuwa kweli watu watazuiliwa kushangilia timu hizo bila Hati ya kusafiria.
“Alichozungumza Waziri (Dk. Ndumbaro) alikuwa anahamasisha uzalendo wa Timu zetu na katika lugha zetu za michezo waandishi wa michezo tunafahamu, Mimi niliwahi kuwa wakati fulani Mwandishi wa Michezo na niliwahi kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo (TASWA) sisi tukizungumza 80% ni utani,  20% tunazungumza vitu vimekaa vimenyooka” amesema Matinyi.
“Ukizungumza habari zinazohusisha Simba na Yanga, ukang’ang’ana kuzungumza kitu kama kilivyoandikwa mahali fulani hivi inafika mahali unawachosha watu, hizi ni timu zinazopenda utani ni timu zinazopokea ujumbe wakati mwingine kwa lugha rahisi, si kweli kwamba Mhe Waziri alimaanisha pale itakaguliwa passport, anayejua passport halali na isiyo halali ni Idara ya Uhamiaji, hakusema Idara ya Uhamiaji itaenda uwanjani pale”
“Kwahiyo katika ushabiki huohuo wa mpira watu wamelifanya jambo hili la mzaha wamelikuza mpaka Mamelodi wamesikia wameingia uoga, na wameandikiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lakini mimi niwasihi Watanzania tuwe Wazalendo na tutarajie Mamelodi watafungwa  magoli mengi na Yanga  na Al Ahly nao watafungwa magoli ya kutosha na Simba" amesisitiza Matinyi.
Ikumbukwe mechi  hizo  kwanza za Robo Fainali Ligi ya Mabingwa Afrika zitachezwa Machi 29 na 30 katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.


source http://www.binzubeiry.co.tz/2024/03/msemaji-wa-serikali-matinyi-afafanua.html

Post a Comment

Whatsapp Button works on Mobile Device only

Start typing and press Enter to search